Moyo kushindwa kufanya kazi (Heart failure) hutokana na ugonjwa wowote wa kimuundo au utendaji kazi wa moyo, unaoathiri uwezo wa moyo kufanya kazi kama pampu ili kusaidia mzunguko wa damu.
Ambapo utendakazi usio wa kawaida wa moyo huchangia kushindwa kwa moyo kusukuma damu kwa kasi inayolingana na mahitaji ya tishu za mwili.
Kufeli kwa moyo kunaweza kusababishwa na kufeli kwa misuli ya moyo (myocardial failure), kufeli kwa moyo husababisha kufeli kwa mzunguko wa damu (circulatory failure).
YANAYOCHANGIA KUFELI KWA MOYO
Kufeli kwa moyo ni hali ya Moyo kushindwa kufanya kazi (Heart failure), sababu ya kawaida ya kushindwa kwa moyo ni pamoja na uhafifu wa mtiririko wa damu kwenye misuli ya moyo (ischemic cardiomyopathy), ikiwemo shida ya kufunga au kutokufunguka vizuri kwa vali ya moyo (Valvular cardiomyopathy).
Maisha ya mjini huchangia kufeli kwa moyo kulingana na viwango vya ugonjwa wa sukari, shinikizo la damu, vyakula vya makopo au vya kusindika na maisha ya kukaa zaidi (sedentary lifestyle).
Walio na umri zaidi ya miaka 75 wapo hatarini zaidi. Hata hivyo, kufeli kwa moyo kunaweza kutokea kwa umri wowote, kulingana na sababu.
AINA TATU ZA KUFELI KWA MOYO
Kuna aina tatu za kufeli kwa Moyo:
(1) Kufeli kwa moyo upande wa kulia (Right-sided Heart Failure) hutokana na udhaifu wa chemba ya kulia ya moyo kushindwa kusukuma damu ya kutosha kwenda kwenye mapafu.
(2) Kufeli kwa moyo upande wa kushoto (Left-sided heart failure) hutokana na udhaifu wa chemba ya Moyo upande wa kushoto haisukuma damu ya kutosha kuzunguka mwili.
(3) Kufeli kwa moyo kwa pande zote mbili (Bilateral cardiac failure) ni hali mbaya ambayo moyo hausukumi damu kwa ufanisi inavyopaswa. Hutokea ikiwa moyo hauwezi kusukuma damu (systolic) au kujaza damu (diastolic) vya kutosha, ambapo pande zote mbili za moyo huathiriwa.
KUFELI KWA MOYO UPANDE WA KULIA
Kufeli kwa moyo upande wa kulia (Right-sided Heart Failure) hutokana na udhaifu wa chemba ya kulia ya moyo katika kusukuma damu ya kutosha hadi kwenye mapafu.
Damu inapoongezeka kwenye mishipa, majimaji husukumwa nje kwenye tishu za mwili na hapo ndipo miguu huvimba. Dalili ni pamoja na shida ya pumzi, kichefuchefu, maumivu na kuvimba kwa tumbo (ascites).
‘Anasarca’ huwa ni kuvimba mwili kwa ujumla ikijumuisha kanyagio, kifundo cha mguu, eneo la mfupa wa chini ya goti (pretibial) na sehemu ya chini ya mgongo (sacral edema).